Katibu na Mwanasheria mkuu wa kampuni ya ufuaji umeme ya IPTL, Bw. Joseph Makandege akiwaonyesha waandishi wa habari (hawapo pichani) nakala ya hukumu iliyotolewa na mahakama kuu ya Tanzania ikizuia benki ya Standard Chartered ya Hong Kong na Tanesco kuendelea kuwabugudhi wamiliki wa IPTL na kuingilia uendeshaji wa mitambo yake. Kushoto ni Meneja Rasilimali watu wa IPTL Bw. Aidan Kaude
Mahakama Kuu ya Tanzania imeiamuru Benki ya Standard
Chartered ya Hong Kong na Shirika la usambazaji Umeme Tanzania (TANESCO) kuacha
kuingilia utulivu, umiliki, usimamizi na utawala wa mitambo ya ufuaji umeme ya
Harbinder Singh Sethi iliyopo Tegeta,na kusubiri uamuzi wa mwisho wa kesi yao
ya msingi.
Hukumu hiyo iliyotolewa jana Dar es salaam na mahakama Kuu
kutoa zuio la kudumu kwa benki ya standard Chartered kuhusu umiliki wa IPTL na
kwamba zuio hilo na PAP ndiye mmiliki halali wa IPTL na siyo wengine wowote.
Akizungumza na waandishi wa habari Mwenyekiti na mtendaji wa
PAP/IPTL,Seth alisema kuwa hukumu hiyo inaeleza kuwa IPTL iendelee kuzalisha
umeme kama ilivyokuwa inafanya na kuwauzia TANESCO huku mmiliki halali akiwa ni
PAP.
“tunapenda kuwakumbusha watanzania kwamba PAP/IPTL
imejizatiti kikamilifu kuhakikisha inawahudumia ipasavyo na kwamba inawataka
wapuuze watu wanaotoa maneno ya uongo ili kuwavuruga utendaji na utoaji huduma
alisema Seth”
Aliongeza kuwa kumekuwepo na maneno mengi yanayotokana na
kutokuwa na uelewa mzuri kwa wanayoyasambaza kutokana na chuki za kibiashara na
mengine yanayotakana na kutafuta sifa za kisiasa,alisema taarifa ambazo
zimekuwa zikitolewa mara kwa mara kuhusu IPTL kuwa na mgogoro na TANESCO
mahakamani siyo kweli na wala hawana shida yoyote mahali popote duniani.
Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited na Pan African
Power Solutions Limited (PAP) zilifungua
kesi kwa kuhoji uhalali wa maamuzi ya kituo cha kimataifa cha kutatua migogoro
ya uwekezaji (ICSID) dhidi ya Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong (SCB-HK)
na Martha Renju anayedaiwa kuwa msimamizi wa mali zake,ijukanayo kama “Decision
on Jurisdiction and Liability” iliyotolewa katika kesi ya ICSID namba
ARB/10/20.Katika hukumu hiyo yenye ukurasa 16 iliyoandikwa na Jaji
Dkt.Fauz Twaib na kusomwa kwa niaba yake
na Jaji Amri Msumi Hamisi, Mahakama Kuu iliwazuia SCBHK au TANESCO kuendelea
kuwabughuzi IPTL/PAP zinazomilikiwa na Seth mpaka pale uamuzi wa mwisho wa kesi
yao ya msingi itapoamuliwa .
Katika hukumu hiyo iliyotolewa na mahakama mbele ya Bw.Sethi
mmiliki wa IPTL/PAP na Kieren Day (Mkurugenzi wa SCB-HK), Jaji Twaibu aliamuru
TANESCO kutofanya biashara yoyote na SCB-HK au Martha Renju kwa niaba ya
IPTL/PAP bila ya kuwa na idhini ya kimaandishi kutoka kwa IPTL/PAP.
“wadaiwa kwa pamoja wanazuiliwa kufanya utekelezaji wa
maamuzi yaliyotolewa katika chombo cha kimataifa ya ICSID yenye namba ARB/10/20
na kusambazwa kwa wahusika February 12,2014 kwa namna yeyote ile na kusubiri
uamuzi wa mwisho wa kesi yao ya madai” inasomeka sehemu ya hukumu hiyo.
TANESCO ambayo iliwakilishwa na wakili wake Urassa, pia
imezuiliwa kutolipa kwa SCB-HK na Martha Renju malipo yoyote wanayostahili IPTL/PAP bila ya idhini ya maandishi kutoka
kwa IPTL/PAP.
Mahakama pia imezuia
TANESCO kutotekeleza au kukubaliana na au kuyatekeleza maamuzi ya ICSID na
kusubiri uamuzi wa mwisho wa kesi yao ya msingi. Jaji Dkt Twaib alitupilia
mbali hoja ya mwanasheria wa SCB-HK,Charles Morrison ambaye alisema kuwa
mahakama Kuu ya Tanzania haipaswi kusikiliza na kutoa maamuzi juu ya ombi hilo
sababu Tanzania ni mwanachama wa kituo cha kimataifa cha kutatua migogoro ya
uwekezaji (ICSID) ambayo pia inajulikana kama Washington Convention au ICSID.
Kwa mujib Jaji Dkt.Twaib, Wakili Morrison alionya kuwa kama Tanzania
haitotii wajibu huo,itajiweka sehemu mbaya katika Nyanja za kimataifa “kwa
heshima kubwa, nashindwa kuona mantiki ya utetezi wa Morisson ya jinsi gani
litaathiri mamlaka ya mahakama hii ya kukubali ombi hili. Japokuwa Morrison
amekwepa kusema moja kwa moja,maoni yake yamelenga kusema kwamba mahakama hii
haina mamlaka ya kutoa amri husika.
“Ninashindwa kuelewa ni jinsi gani Serikali ya
Tanzania,ambayo ni sehemu ya kesi hii,itakuwa imevunja mkataba wa Washington
kwa sababu wananchi wake wawili ambao ni wafanyabiashara binafsi wametafuta
amri ya kuzuia utekelezaji wa ICSID kwa misingi ya udanganyifu. Sioni ni jinsi
gani,kwa kutumia mamlaka yake katika kutoa maagizo yao mamlaka itakuwa
inaingilia majukumu ya kimataifa ya Tanzania chini ya mkataba wa Washington
inasomeka hukumu ya Jaji Twaib.
Sababu ya pili ya Bw.Morissin ya kuona mahakama isikubali
ombi hilo ilikuwa kwamba madai hayo yanaweza kuwa yametolewa miaka mingi
iliyopita wakati kesi ya ICSID ilipoanza na kubainisha kuwa hii ni kesi
iliyokufa (tort case) ingekuwa imefanyiwa kazi ndani ya miaka mitatu ya tarehe
ile ile.
Jaji Twaib alitupilia mbali hoja hiyo kwa kusema “kwa
heshima kubwa kwa Bw.Morrison hoja hii haina nguvu ya kisheria.kama ilivyosemwa
na Mwanasheria wa waombaji (Bw.Joseph Makandege na Bw.Melkezedek Lutema) madai
hayo yanatoa changamoto kwa uamuzi wa ICSID ambayo ulitolewa mwezi
Februari,2014,haiwezi ukasemwa imepitwa na wakati .Ninatupilia mbali pingamizi
hilo”
Kuhusu ombi kuwa shauri hilo lisikilizwe katika mahakama ya
Hong Kong na fedha zote zipelekwe huko,wanasheria wote, Makandege na Lutema
walisema litakuwa si kutenda haki kwa mteja wao,kwakuwa kuna kiasi kikubwa cha
fedha kinahusika,ambayo itakuwa vigumu kuirejesha na kuwa itakuwa vigumu kwa
IPTL/PAP kurejea katika hali yake kwa sababu SCB-HK ni ya nje na haina mali
zozote kubwa Tanzania.
SOURCE: GAZETI LA MAJIRA TAREHE 02,OCTOBER,2014
PICHA:KWA HISANI YA TANZANIA DAIMA
Hongera sana IPTL !!
ReplyDeleteTUNAFAHAMU MWISHO WA KAFULILA NI KUUMBUKA NA SISI WANAKIGOMA KUSINI TUNAMSUBIRI KWA HAMU KUBWA 2015