KARIBU SANA

Monday, 13 October 2014

IPTL YAIGALAGAZA STANDARD CHARTERED MAHAKAMANI













Na Mwandishi Wetu

MAHAKAMU Kuu ya Tanzania, imekataa maombi ya Benki ya Standard Chartered ya Hongkong dhidi ya Kampuni ya IPTL kutokana na maombi yao kutokidhi mahitaji ya kisheria.

Uamuzi wa mahakama hiyo, ulitolewa na Jaji wa Mahakama hiyo, Salvatory Bongole alisema anayatupa maombi hayo kwa dhidi ya Kampuni hiyo kwa kuwa yamekosa uhalali wa kisheria japokuwa maelezo yao yanavutia.

Benki hiyo iliomba Mahakama Kuu isisikilize kesi hiyo hadi pale washitaki watakapoweka sh. bilioni 787 kama gharama ya kesi hiyo dhidi ya ya kampuni ya IPTL

“Nina kiapo cha (Wakili Gasper) Nyika na nyaraka alizowasilisha ingawa zinavutia lakini zimekosa uhalali wa kisheria,na hivyo ninayakataa maombi haya” alisema Jaji Bongole.

Uamuzi wa Mahakama ulitokana na upande wa utetezi kushindwa katika maombi yao, mahakamani hapo kuwekewa malipo ya fedha za gharama kabla ya kusikilizwa kesi hiyo dhidi ya IPTL.

Kwa mujibu wa Jaji Bongole alisema kulikuwa hakuna ushahidi uliotosheleza kuonyesha kuwa kampuni ya VIP haina mali nyingine zinazoweza kufikia gharama za kesi dhidi ya mlalamikaji endapo ataibuka mshindi katika kesi kuu.

Jaji Bongole alisema maombi hayo yanaweza kukubaliwa kwa hiari ya mahakama, baada ya kujiridhisha kuwa mlalamikiwa hana uwezo wa kulipa gharama hizo baada ya kushindwa kesi.

Katika maombi yake, Wakili Nyika alitoa hoja kuwa Kampuni ya VIP ilikua inategemea 30% ya hisa zake ndani yake ya kampuni ya IPTL ambazo zimeuzwa na suala lake kisheria liko kwenye amri ya mahakama.

Jaji alisema kuwa baada ya kupitia hoja iliyowasilishwa amegundua kuwa hisa hizo bado zipo na hakuna uthibitisho kuonesha kuwa VIP haina rasilimali ya kulipa gharama hizo, wakati wa kusikiliza maombi hayo Kampuni ya VIP iliwakilishwa na na timu ya mawakili wakiwemo Cathbert Tenga, Michael Ngalo, Respicious Didace, Okare Emesu na Herin Manento.

Mawakili hao walidai faraja iliyokuwa ikitafutwa na walalamikaji haikuwa na mashiko kisheria na hoja zote zilizowasilishwa kortini ni sawa na kutuhumu mahakama dhidi ya VIP kwa kutokua na uhakika pamoja na kutoa maamuzi ya hukumu ya kesi hiyo kabla haijaisha.

Kwa mujibu wa mawakili, walalamikaji waliwasilisha ombi hilo kwa makusudi na kuvuruga mchakato wakiwa na lengo la kuchelewesha mchakato wa mahakama kutoa hukumu ya madai halali ya mlalamikiwa.

Baada ya ombi hilo kukataliwa, Jaji aliagiza kuanza kusikilizwa kwa kesi kuu kwa mara ya kwanza kabla ya hukumu 6 Novemba, mwaka huu,ili kujiridhisha kama pande zote mbili zimewasilisha utetezi wao kabla ya kuanza majadiliano.

Kampuni ya VIP imezishitaki kampuni zote zilizowasilisha malalamiko pamoja na kampuni nyingine mbili Wartsila Nederland BV na Wartsila Tanzania Limited wakizidai Dola za marekani milioni 490.9 kwa udanganyifu, kuhamisha haki zake,na kuchafua kampuni yake na maslahi yake ndani ya IPTL.

Katika shitaka hilo mbali na kudai fidia ya fedha, Kampuni ya VIP inataka tamko kwamba kampuni yake na IPTL imepata hasara kubwa kutokana na tabia na vitendo vya walalamikiwa.

Mlalamikaji pia anataka mahakama itamke kwamba hakuna Benki wala wakala aliye mkopeshaji halali wa IPTL na kwamba walalamikiwa wamekuwa wakifanya udanganyifu, utakatishaji fedha, kuchafua kampuni, na unyonyaji, uhamishwaji fedha, na uhamishwaji wa mali za IPTL na VIP kama matokeo ya vitendo vyao.

Pia kampuni ya VIP imeitaka mahakama kuiagiza kampuni ya Wartsila kuendesha mradi wa gesi na mafuta mazito kwa ajili ya mradi wa Kampuni ya IPTL kwa gharama zisizozidi dola za marekani milioni 11.5 .

Kampuni ya VIP ilikua mmiliki wa asilimia 30 za IPTL wakati kampuni ya Mechmar ikimiliki asilimia 70, ambapo sasa kampuni hiyo inamilikiwa na kampuni ya PAP, baada ya kuinunua kampuni hiyo.

SOURCE: MAJIRA,HABARI LEO,NA JAMBO LEO

No comments:

Post a Comment